Kikombe cha ushindi katika maonyesho ya nane nane ambacho kampuni ya maziwa ya Asas ilipata |
Wananchi Dodoma wakiwa katika banda la Asas wakati wa nane nane kununua maziwa |
Nyani aliyekuwepo katika maonyesha wakulima nane nane katika mikoa ya nyanda za juu kusini mkoani Mbeya akifurahia maziwa ya Asas |
Na Francis Godwin
KAMPUNI ya Asas Dairies Ltd ya mkoani Iringa imeibuka kidedea baada ya kushinda tuzo katika maonyesho ya wakulima nane nane mkoani Arusha na Mbeya. Pia kampuni hiyo imeeleza kufurahishwa sana na mwitikio mkubwa wa wananchi ambao walikuwa wakifuruka katika mabanda yao kupata maelezo na kununua maziwa hayo, ikisema kuwa hilo ni jambo la kujivunia.
Asas Dairies Ltd yenye makao yake makuu mkoani Iringa mbali ya kushinda tuzo hizo pia ndio kampuni iliyoshinda tuzo ya ubora wa maziwa Tanzania kati ya makampuni 30 yaliyoshiriki mashindano mwaka huu na mwaka jana .
Akizungumzia ushindi wa kampuni hiyo Ritta Mlagala ambae ni mmoja kati ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa ambao waliofika katika maonyesho ya nane nane jijini Mbeya na kufika katika banda hilo alisema kuwa umefika wakati wa watanzania kupenda bidhaa zetu wenyewe. Alisema kuwa ubora wa maziwa hayo na ushiriki na kushinda kwa kampuni hiyo katika maonyesho mbali mbali ni heshima kubwa kwa mkoa wa Iringa .
“Kuongoza katika nafasi zote zilizoshindaniwa si jambo dogo ni jitihada kubwa zimefanyika na ni hatua ya kujivunia kwa kampuni hiyo. ” alisema na kuongezea: “Imani ya watumiaji wa maziwa imekuwa ikiongezeka zaidi hasa pale kampuni inapoendelea kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali”.
Kwa upande wake afisa masoko wa kampuni hiyo ya Asas Dairies Ltd Jimmy Kiwelu alisema kuwa mbali ya kampuni hiyo kuongoza kwa mwaka huu bado ilipata kuongoza katika mashinadano kama haya yaliyofanyika mwaka jana mkoani Ruvuma na kuwa lengo la kampuni ni kuendelea kuongoza daima na kuzidisha ushiriki wake katika maonyesho ya nane nane na yale ya saba saba
Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na bodi ya maziwa Tanzania( TDB) jumla ya makampuni 30 yalishiriki ikiwemo kampuni ya Tanga fresh,Musoma Dairies,Kilimanjaro creamer,Engingten,Arusha,Ammy Dairies Njombe cefa,Victoria dairies ,Uvingo dairies na mengine mengi kampuni ya Asas Dairies iliweza kuibuka na ushindi wa jumla baada ya kushinda tuzo zote tatu zilizokuwa zikishindaniwa na hivyo kufanikiwa kuondoka na tuzo nne zote ikiwemo ya mshindi wa jumla.
Kiwelu aliwataka watanzania kuendelea kuzipenda bidhaa za Asas Dairies Ltd kutokana na kuendelea kuongoza katika ubora na kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuona ubora huo unaendelea zaidi na kila mwaka kuendelea kufanya vema. Pia alipongeza watanzania na watumiaji wa bidhaa za Asas Dairies Ltd kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa kuendelea kutumia maziwa yanayozalishwa na kampuni hiyo ya Asas Dairies Ltd Iringa